Tuesday, November 6, 2012

KORTINI KWA RUSHWA



AFISA MTENDAJI, MAWAKALA WA PEMBEJEO KORTINI KWA RUSHWA

                     Na  Bazil   Makungu Ludewa

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa wilayani Ludewa katika Mkoa mpya wa Njombe imemfikisha mahakamani kwa makosa kumi na tatu ya rushwa na udanganyifu Yohana Jenkin Pili (50)afisa mtendaji wa kijiji cha Kipangala kilichopo katika kata ya Luilo Ludewa.

Pamoja naye wengine waliofikishwa katika mahakama hiyo ya hakimu mkazi Ludewa mjini ni pamoja na Kilian Kilian Mbawala (40) mwenyekiti wa kamati ya pembejeo na Sebastian Haule(26) mkazi wa Ludewa mjini ambaye ni wakala wa mbolea katika kijiji cha Kipangala.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Fredrick Lukuna hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya Ludewa, mwendesha mashtaka wa Takukuru Restituta Kesi aliiambia mahakama kuwa washtakiwa wote kwa pamoja walitenda makosa hayo june mwaka huu.

Kesi akaongeza kuwa Sebastian Haule kwa akishirikiana na wenzake Yohana Jenken Pili na Kilian Kilian kati june 2011 na 2012 walitoa rushwa na kuwasainisha vocha za pembejeo wananchi zaidi ya 13 wa kijiji cha Kipangala kwa malipo ya shilingi 20,000 (shilingi ishirini elfu) kila mmoja bila kuwapa pembejeo.

Mwendesha mashtaka akaongeza kuwa makosa yote yanaangukia chini ya kifungu 15(ii)(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa no 11 ya mwaka 2007, hata hivyo washtakiwa wote walikana kuhusika na makosa yanayowakabili hata hivyo upelelezi wa kesi hizo umekamilika.

Akitoa masharti ya dhamana hakimu Lukuna akasema dhamana iko wazi kwa washtakiwa na kwamba kila mmoja atatakiwa kudhaminiwa na mdhamini mmoja kwa thamani ya jumla ya shilingi 1milioni kilka mmoja au mali isiyohamishika.

Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana na kesi kuahirishwa hadi novemba 21 mwaka huu kesi itakapokuja kwa kusikilizwa kwani upelelezi wa shsuri ulikwisha kamilika.

Katika kesi nyingine ya udanganyifu katika pembejeo mahakama ya hakimu mkazi wilayani Ludewa imemwachia huru Afisa mtendaji wa kijiji cha Mdilidili kata ya Lugarawa Bw Kayombo Komnfoti na wenzake baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa yanayowakabili.
                   mwisho

No comments:

Post a Comment