Tuesday, July 2, 2013

MWENYEKITI AFUNGWA JELA MIAKA SITA KWA RUSHWA.





Na Bazil Makungu

MWENYEKITI wa kijiji cha Mbugani kata ya Mavanga wilaya ya Ludewa katika Mkoa wa Njombe Ignas Mgaya amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka sita jela au kulipa faini ya shilingi milioni moja na nusu(1,500,000) baada ya kupatikana na hatia ya kushawishi na kupokea jumla ya shilingi 50,000 kutoka kwa mlalamikaji.

Mbele ya Fredrick Lukuna,Hakimu mkazi mfawidhi katika mahakama ya wilaya ya Ludewa mshitakiwa akatiwa hatiani baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Awali mwenyekiti huyo wa kijiji alishtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kosa la kushawishi na kupokea hongo ya shilingi 50,000 kutoka kwa Bw Philmoni Mlelwa makosa yanayoangukia chini ya kifungu namba 15 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takribani masaa mawili Mh, Lukuna alisema ushahidi wa upande wa utetezi haukuleta mahakama ushahidi wa vikao vyenye mihutasari vilivyofanyika wakati wa kutatua migogoro ya ardhi iliyokuwa ikitatuliwa kati ya Bw Benson Mtweve na Philimon Mlelwa.

Naye mwendesha mashtaka wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU) Restuta Kessy kwa upande wake akaiambia mahakama kuwa pamoja na kwamba hana kumbukumbu za makosa ya nyuma kwa mshtakiwa akaiomba mahakama kutoa adhabu kali ili liwe fundisho kwa watumishi wasio waadilifu.

Akitoa hukumu hiyo Lukuna akasema makosa kama haya yamekuwa mengi katika jamii yetu na kwamba wananchi wamekuwa wakikosa haki zao na wakati fulani kunyonywa kwa kisingizio cha kutojua sheria, sasa ili liwe fundisho kwa mshtakiwa na kwa wale wanaojiandaa makosa kama haya mahakama inatoa amri.

Kwa kuwa Mshtakiwa anashtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kushawishi na kupokea fedha ya shilingi 50,000 mahakama inatoa amri ya kulipa faini ya shilingi 750,000 kwa kila kosa ambapo kwa makosa yote mawili mshtakiwa atatakiwa kulipa jumla ya shilingi milioni 1.5 au kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa kama atashidwa kulipa faini. Hata hivyo mshtakiwa alilipa faini na kuachiwa.

Wakati huohuo kesi ya kuomba na kupokea rushwa inayomkabili afisa mtendaji wa kata ya mlangali Edward Makamba Matalawasula imeahirishwa hadi Augost 2 mwaka huu iatakapo kuja kwa kusikiliza mashahid.

                        mwisho







 

No comments:

Post a Comment