Na
Bazil Makungu Ludewa
SERIKALI
kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa inatakiwa kuharakisha mpango
wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yote yaliyomo ndani na nje ya
migodi ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kutokana na ongezeko
la watu wanaotarajia kuingia kufuatia machimbo na migodi ya makaa ya
mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga inayotarajia kuanza muda mfupi
ujao.
Kauli hiyo
imetolewa na Wananchi wa kijiji cha Nindi kata ya Lupingu Ludewa
Mkoani Njombe katika kikao cha kuanisha mipaka ya matumizi mbalimbali
ya ardhi kijijini hapo iliyopendekezwa na kamati maalum na wataalamu
kutoka halmashauri ya wilaya taarifa iliyopokelewa kwa furaha na
halmashauri ya kijiji hicho (VC) kabla ya kufikishwa kwenye mkutano
wa hadhara wa wananchi wote.
“”” tuna
hofu ya kutokea kwa migogoro mikubwa katika maeneo yetu kama serikali
itachelewa kukamilisha mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa wilaya
yote ya Ludewa kwa sababu sisi wenyewe tunagombana wageni wanaokuja
kwenye migodi ni wengi, inatakiwa waje wakute ardhi ilishapangiwa
matumizi na watu wawe wamepewa hati za kimila.””” alisisitiza
mzee Henjewele
Katika
kijiji hicho maeneo mbalimbali ndani vitongoji vya Nindi juu, Nindi
kati, Njelela na Ipombo yaliainishwa ikiwemo ardhi itakayotumika kwa
kilimo, malisho ya mifugo, makazi ya watu, misitu ya hifadhi, vyanzo
vya maji, huduma za kijamii na ardhi ya akiba kwa matumizi ya
baadaye.
Wananchi kwa
upande wao wameishukuru halmashauri ya wilaya ya Ludewa pamoja na
timu ya wataalamu kwa kufikisha mpango huo kwa wakati na kwamba kwao
ni ukombozi kwa sababu ndugu , jamaa na marafiki wamekuwa wakiishi
kwa uhasama kutokana na ugomvi wa ardhi ambao umekuwa ukitokea mara
kwa mara na kupoteza muda ambao wangeutumia kwa maendeleo badala yake
wamekuwa wakishinda kwenye mahakama kutafuta haki.
Akizungumza
katika mkutano huo Afisa ardhi mteule katika halmashauri ya wilaya ya
Ludewa Joseph Kamonga alisema kufuatia mpango huo wa matumizi bora ya
ardhi serikali itatoa hati miliki za kimila kwa wananchi ambazo
huongeza usalama wa miliki kwa sababu hati ni ulinzi uliopo kisheria.
Kamonga
alizitaja faida zingine za hati miliki ya kimila kuwa ni pamoja na
kupunguza migogoro ya ardhi, hati kutumika kama dhamana ya mikopo na
fedha katika taasisi za fedha kama benki ya raslimali, kuongeza
thamani ya ardhi, kutumika kama dhamana mahakamani na nu utii na
utekelezaji wa sera ya Taifa ya ardhi ya mwaka 1995 na sheria za
ardhi.
Kamonga
akaongeza kuwa halmashauri ya wilaya ya Ludewa inatekeleza mradi huu
kupitia akaunti ya miradi ya maendeleo fedha iliyoidhinishwa na
baraza la madiwani kwa ajili ya vijiji vya Iwela katika kata ya Iwela
na kijiji cha Nindi katia kata ya Lupingu.
Aidha
akaipongeza Mkurabita kwa kugharamia vijiji viwili vya mfano kikiwemo
kijiji cha Amani na Lifua pamoja na kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo
madiwani na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa kuhusu
mpango wa matumizi bora ya ardhi pia kugharamia na kuleta vifaa
mbalimbali vya kupimia ardhi kama GPS kumi (10) na komputa tatu (3)
ambavyo vinasaidia kurahisisha kazi.
Akizungumza
na gazeti hili katibu wa mbunge wa Ludewa Stanley Gowele alisema
mwaka 2014 wafanyakazi 2700 wa kudumu katika migodi wanatarajia
kuingia wilayani Ludewa ambapo kati yao 2000 watakuwa kwenye chuma
cha Liganga na 700 watakuwa mchuchuma.
Mwaka 2015
wataingia wafanyakazi 3000 kati yao 2000 watakuwa Liganga na 1000
watafanyakazi kwenye mitambo ya kuzalisha umeme mchuchuma, mwaka 2016
Ludewa inatarajia kupokea wafanyakazi 3500 ambapo 1000 watapelekwa
mchuchuma na 2500 watakuwa Liganga, mwaka 2017 wafanyakazi wataingia
4500 ambapo mchuchuma watakuwa 1500 na Liganga 3000 na mwaka 2018
Ludewa inatarajia kupokea wageni 7000.
Kwa mujibu
wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agost 2012 wilaya inajumla ya
wakazi 128,155 kati yao wanaume ni 60,477 na wanawake 67,678 wastani
wa ongezeko la watu kwa mwaka ni 1.6% hadi kufikia 2012 na sasa
wilaya ya Ludewa inakadiriwa kuwa na watu 152, 285 kati yao wanawake
79,318 na wanaume ni 72,968 ambapo kiutawala wilaya ya Ludewa
imegawanyika katika tarafa 5 kata 25 vijiji vilivyoandikishwa 77 na
vitongoji 340.
Wilaya ya
Ludewa ina eneo la kilomita za mraba 8,397 kati ya hizo kilomita za
mraba 73.54 ni hifadhi ya misitu, kilomita za mraba 2,072 ni maji na
milima na kilomita 6,251.46 zinafaa kwa makazi ya watu na kilimo.
mwisho
No comments:
Post a Comment