Friday, November 30, 2012

MKUU WA MKOA ASITISHA ZIARA MWAMBAO WA ZIWA NYASA NI BAADA YA ZIWA KUCHAFUKA GHAFLA.



MKUU WA MKOA  ASITISHA ZIARA MWAMBAO WA ZIWA NYASA NI BAADA YA ZIWA KUCHAFUKA GHAFLA.

                 Na Bazil Makungu

MKUU wa mkoa wa Njombe Captain mstaafu Aseli Msangi amelazimika kukatisha ziara yake katika tarafa ya mwambao wa ziwa nyasa wilayani Ludewa baada ya ziwa kuchafuka ghafla kwa dharuba na mawimbi makali.

Msangi alikumbwa  na mabadiliko hayo baada ya kumalizika mkutano wa hadhara katika kijiji cha makonde novemba 27 ambapo kwa mujibu wa ratiba baada ya mkutano huo alitakiwa kwenda kufanya mkutano kama huo kata ya Lifuma kwa njia ya boti na kulala hapo.

Kutokana na ziwa hilo kuchafuka ghafla ndipo msafara ukasimama kwa muda kusubiri kama dhoruba ingepungua lakini haikuwezekana na ndipo mkuu huyo wa mkoa akalazimika kuachana na boti na kuamua kutembea kwa mguu kwa takribani masaa matatu kutoka makonde hadi kata ya Lifuma .

Hata hivyo Msangi wakati Fulani alilazimika kutumia maneno makali na kutoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha makonde kufuatia baadhi ya kikundi cha watu wachache wanaojiita kambi ya kaboya kutaka kudhoofisha mkutano huo kwa kubandika mabango ya kumtaka aondoke na diwani wao kwa madai kuwa yeye ni fisadi taarifa ambazo hata hivyo walishindwa kuthibitisha na ikaonekana ni majungu ya kutotaka kufanyakazi.

 Msafara kata ya Lifuma ukapokelewa vizuri kwa ngoma za mganda na Ligambusi na shangwe zaidi kuliko ilivyokuwa kata ya makonde ambako baadhi ya watu wachache waliandaa mabango ya kumtaka mkuu huyo kuondoka na diwani wao.
Mabango hayo yalikuwa yakimtuhumu diwani Cricypin mwendapole Mwakasungura kwa ufisadi lakini hakuna aliyejitokeza kuthibitisha ufisadi wa diwani huyo ndipo wakatakiwa kufuata sheria badala ya kuendekeza majungu huku wakichelewesha maendeleo yao wenyewe.

Aidha mkuu huyo akalazimika kukaa Lifuma siku mbili mfululizo kusubiri ziwa kupungua dhoruba lakini haikuwezekana na ndipo novemba 29 mwaka huu akalazimika kutembea tena kwa mguu masaa mawili kutoka Lifuma mpaka kijiji cha cha Nsisi ambapo alipanda boti kurudi kata ya makonde na kusafiri kwa magari ya paroko hadi Ludewa mjini.

Katika ziara hiyo mkuu wa mkoa wa njombe capteni mstaafu Aseli Msangi alipita kuhamasisha na kukagua shughuli za maendeleo na kuwaondoa hofu wananchi katika mwambao huo kuhusu mgogoro wa mipaka unaoendelea kati ya Tanzania na Malawi.

Juma Madaha Ratiba ya siku tatu ziara ya mkuu huyo ilianza jumatatu novemba 25 mwaka huu kwa kupokea taarifa ya wilaya katika ofisi ya mkuu wa wilaya Ludewa Juma Mahaha na kufuatiwa na mkutana wa hadhara katika kata ya Lupingu.

Baada ya mkutano huo uliojaa vijembe na kiburi cha kumtaka diwani aendolewe kienyeji kumalizika na msafara kutakiwa kuondoka kuelekea kata ya Lifuma ndipo ghafla ziwa likachafuka na kulazimika kutembea kwa mguu.
Aidha mkuu wa mkoa alilazimika kulala siku mbili katika kasiri ya kanisa katoliki kutokana na ziwa hilo kuendelea kutishia usalama wa msafara huo ambapo kila kukicha mawimbi yalikuwa yakiongezeka na kupelekea kushindwa kuendelea na ziara.

Akitoa ratiba ya ziara mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha aliliambia gazeti hili kuwa novemba 28 mkutano wa hadhara ulitakiwa kufanyika kata ya Kilondo na 29 kata ya Lumbila na na kisha kuunganisha hadi Matema Kyela mkoani mbeya lakini ilishindikana kutokana na kuongezeka kwa dhoruba.

Hata hivo Madaha akaongeza kuwa ziara imesitishwa hadi desemba 12 mwaka huu ambapo sasa ziara itaanzia kyela na kuzifia kata ya Lumbila na Kilondo. 

Mkuu wa mkoa pamoja na mambo mengine alipita kuzungumza na wananchi pia kuwaondoa hofu kufuatia mzozo na mvutano wa mipaka unaoendelea kati ya Tanzania na Malawi.

Aidha msangi amewataka wananchi wa mwambao wa ziwa nyasa kujiondoa katika wimbi la umaskini kwa kutengeneza mizinga ya nyuki kwa sababu haihitaji pembejeo wala kuchonga mitumbwi.

Tarafa ya mwambao wa ziwa nyasa ina kata za Lupingu, Ilela, Lifuma, Kilondo na Lumbila ambazo wananchi wake wanategemea uvuvi duni wa samaki kuendeshe maisha yao ya kila siku.
              mwisho



No comments:

Post a Comment