Na.Bazil Makungu,Ludewa.
WANANCHI wa kata ya Ludewa wilayani Ludewa
katika Mkoa wa Njombe wametishia kugoma kushiriki katika shughuli za maendeleo kama
watakosa pembejeo ya mwaka huu kufuatia vocha kuletwa chache na ugawaji wa
pembejeo hizo kugubikwa na mizengwe ikiwemo upendeleo na vocha hizo
kuletwa chache na kutokutoshereza kwa
wakulima.
Mzozo huo ulizuka katika mkutano wa hadhara
ulioitishwa maalum jana kwa ajili ya kugawa vocha za ruzuku ya kilimo katika
kata ya Ludewa ambapo ilionekana kaya ni nyingi kuliko vocha na kuonekana kuwa
wakulima wengi wenye uwezowa kufanyakazi watakosa.
Awali afisa mtendaji wa kijiji cha Ludewa mjini
Alfredi Mgimba alisema kuwa uchache wa vocha hizo utasababisha uhasama kati ya
wananchi na viongozi wa mitaa na vijiji kwa sababu zimeletwa chache hivyo
kushindwa apewe nani na yupi akose.
’’’ kutokana na uchache huo wa vocha za ruzuku
ya kilimo ofisi imeamua kuitisha mkutano wa hadhara ili wananchi waamue wenyewe
namna bora ya kugawana ili kuondoa manung’uniko hata hivyo tunakusudia
kuwaachia wenyeviti wa vitongoji walete majina ya wananchi wenye sifa za kupewa
vocha’’’ alisema Mgimba
Naye Afisa
mtendaji wa kata ya Ludewa Bw.Onesmo Haule aliwaambia wananchi kuwa kata ya
Ludewa imeleta jumla ya vocha za pembejeo ya kilimo 1061 wakati kata ina jumla
ya kaya 2552 zimegawanywa kwa vijiji viwili ambapo kijiji cha Ludewa mjini
chenye kaya 1752 kimepewa vocha 650 Kijiji cha Ludewa (K) chenye kaya 800
kimepewa vocha 411.
Baada ya kutoa taarifa hiyo ndipo hasira zilipoibuka
kwa wananchi na kuhoji nani atapata na nani atakosa ruzuku hiyo na kwa vigezo
vipi na kuilaumu Serikali kwa kuwarubuni kwa sera ya kilimo kwanza wakati sera
hiyo haitekelezeki.
Bw.Haule aliwasihi wananchi kutokuwa na jazba
kwa tukio hilo na kuahidi kulifuatilia kwa karibu ili kuona kama utatuzi wa
adha hiyo ya pembejeo za kilimo utawezekana kama wananchi wengi walivyo
tarajia.
Aidha Afisa mtendaji huyo aliitupia lawama
Serikali kwa kuwatumia mawakala kusambaza pembejeo hizo badala ya makampuni
kama ilivyotarajiwa na wakulima walio wengi ambapo ingeweza kupunguza bei za
pembejeo hizo.
Bw.Haule alisema Serikali ilipaswa kupeleka
fedha za ruzuku hiyo viwandani na kuyakabidhi makampuni kusambaza kwa wakulima
na si mawakala ambao wamekuwa ni tatizo kila mwaka hali ambayo hudhorotesha
sekta ya kilimo nchini.
“Tumeshangazwa na mfumo huu ambao tumekuwa
tukiupigia kelele kila mwaka kwani hauna tija kwa wakulima zaidi ya
kuwakandamiza wakulima wa hali ya chini kwa kuwaletea vocha chache ili
kuuendeleza umaskini nchini zaidi ya kupunguza”,alisema Bw.Haule.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine
Bw.Alen Msigwa alisema Serikali haina nia ya kuwainua wakulima zaidi ya
kuwakandamiza na Sera ya kilimo kwanza haina tija kwa wakulima wa ndani labda
wakulima wan je walioko nchini.
Bw.Msigwa alisema wananchi waliahidiwa kupewa
pembejeo za ruzuku ikiwapo mbolea ya kupandia mazao na mbegu mapema kabla mvua
kuanza kunyesha lakini suala hilo limekuwa kitendawili hasa wilayani Ludewa
kwani mbegu na mbolea hizo zimefika wakati wananchi wameshapanda mazao.
Alisema vocha hizo hazitoshi na kunahatari
kusababisha mgawanyiko wa wananchi kwani watakaopata vocha hizo ndio
watakaochangia shughuri za maendeleo hivyo itawawia vigumu wenyeviti wa mitaa
kukusanya michango ya maendeleo kwa wananchi wasiopata vocha.
“huku ni kusababisha matabaka miongoni mwa jamii
kwani ni kazi ngumu kuwachagua wakulima kuwa nani apate na naniasipate kutokana
na hali hii sasa tunaamini Serikali haina haja ya kutekeleza sera ya kilimo
kwanza kwani dalili tunaziona na kama haiwezekani watoe taarifa na si
kuwarubuni wananchi”,alisema Bw.Msigwa.
Kutokana na hali hiyo Afisa mtendaji wa kata
Bw.Haule aliwataka wenyeviti wa mitaa kukaa na wananchi wa mitaa yao ili
kupitisha majina ya watakaopata pembejeo hizo ingawa zimechelewa na
hazitoshelezi kulingana na uwingi wa wakulima wa zao la mahindi wilayani
Ludewa.
Bw.Haule aliusukumia mzigo huo kwa wenyeviti wa
mitaa ambao kwa pamoja walisema wafanyakazi walioajiriwa katika ofisi yoyote
hawatapata ruzuku hiyo wakiwemo wakulima wanaojiweza ili kupunguza mgogoro
lakini waliosomwa kutopata waliapa kutotoa michango ya maendeleo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment