Friday, January 11, 2013

NGOYE, FILIKUNJOMBE, WAVALIA NJUGA TATIZO LA MAWASILIANO MWAMBAO WA ZIWA NYASA.




               Na  Bazil Makungu Ludewa
WABUNGE Hilda Ngoye viti maalumu mbeya mjini na Deo Filikunjombe wa jimbo la Ludewa katika mkoa wa Njombe wamesema mateso wanayoyapata watanzania waishio mwambao wa ziwa nyasa sehemu ya Ludewa kuhusu mawasiliano lazima yamepatiwa ufumbuzi haraka ili waweze kuimba kwa pamoja wimbo wa dunia ni kijiji.

Wabunge hao kwa pamoja waliyasema hayo hivi karibuni walipokutana katika kijiji cha Nsisi kilichopo kata ya Lifuma mwambao wa ziwa nyasa Ludewa ambapo Filikunjombe alikuwa katika ziara ya wiki mbili akitembelea, kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo katika vijiji na vitongoji vya tarafa ya mwambo wa ziwa Nyasa na kujionea adha na changamoto zinazowakabili wananchi hao hata baada ya miaka hamsini ya uhuru.

Kwa upande wake Hilda Ngoye ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Nsisi mwambao wa ziwa nyasa akiwa katika likizo fupi ya mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka alipopata fursa ya kuhudhuria mkutano wa mbunge wake Filikunjombe katika kijiji hicho alisema ifike mwisho tuseme sasa wananchi hawa wapate uhuru kwa vitendo kwani tatizo linalowakabili kabla ya uhuru na baada ya uhuru ni mawasiliano ya simu, usafiri wa barabara na adha ya usafiri wa majini.

Ngoye alimwambia Filikunjombe kuwa kizuizi kikubwa cha maendeleo katika mwambao wa ziwa nyasa ni mawasiliano ya simu, barabara, usafiri wa majini na umeme vitu vyote hivi kama vitakuwepo katika mwambao wa ziwa nyasa mwambao utatamanika.

Wakisoma risala kwa mbunge wao wananchi wa kijiji cha Nsisi Kata ya Lifuma walisema wao kila kukicha ni afadhari ya jana kwa sababu hakuna jambo lililo na unafuu na hakuna kitu kinachoweza kuwafanya wafurahie na kunufaika na matunda ya uhuru wao wamebaki gizani tu na kwamba hadi leo wanatumia mawasiliano ya barua ambayo huwachukua miezi kupata majibu.

‘’’’’ ukiangalia usafiri wa meli hakuna uhakika wala ratiba kamili ya meli yetu Mv Songea ambayo hata hivyo imechakaa, meli hiyo inafannya safari usiku jambo ambalo ni hatari sana,usafiri wa barabara huo ndiyo kabisa hakuna anayeshughulika nao, suala la mawasilano ya simu ni kero kubwa mambo haya yote yanafanya maendeleo yetu kubaki yamesimama huku wenzetu wakikimbia’’’’ alisema mwakasungura diwani wa Makonde

Wakizungumza na gazeti hili lililofanya ziara katika mwambao wa ziwa nyasa kujionea changamoto zinazowakabili wananchi waishio vijijini walisema kutokana na kukosa mawasiliano ya simu wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi ikiwemo akina mama kujifungulia njiani wakielekea kwenye vituo vya kutolea huduma na wengine kupoteza maisha.

Kata zinazotajwa kukabiliwa na changamoto ya kukosa mawasiliano na kusahaulika na watendaji wa serikali kiasi cha kupelekea kukosa huduma na mahitaji muhimu ya kibinadamu ni pamoja na kata Kilondo, Lumbila kwa baadhi ya maeneo, Makonde, Lifuma, Iwela na kata ya Lupingu.

Naye mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe alisema mateso ya wananchi waishio mwambao  yamepatiwa ufumbuzi wa kudumu na kwamba katika kipindi kifupi kijacho atahakikisha mawasiliano ya simu yanaanza ili iwe ukombozi kwa mwambao huo ambapo wamekuwa wakibaki nyuma kimaendeleo kwa kukosa mawasiliano ya simu za mkononi. 

“Ndugu wananchi poleni na mateso mnayoendelea kuyapata ndani ya miaka hamsini ya uhuru mimi mwenzenu niliomba minara mitano ya simu serikalini nikapata mitatu na kati ya hiyo nitahakikisha minara miwili inajengwa mwambao wa ziwa nyasa kati ya kata ya Lupingu na Kilondo ili kuungana na ile ya kyela”,alisema Filikunjombe.

Filikunjombe alisema tayari alikwishaomba minara  mitano UCF lakini akapewa mitatu na kwamba miwili atahakikisha inafungwa katika Tarafa ya mwambao na kuongeza kuwa itasaidia wananchi waishio huko kuwasiliana na ndugu na jamaa wa maeneo mengine pia kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kama kutakuwa na wageni wasiofahamika.

Filikunjombe aliwataka wananchi kuwa na subira kwani wataalamu wa minara watakuja kuangalia ni maeneo yapi mazuri yanayofaa kuijenga minara hiyo ili kupunguza kero zinazowakabili ikiwemo katika Afya ambapo wagonjwa wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika kwa kutumia simu za mkononi kuita usafiri.

Akizungumzia barabara ya Ludewa hadi Lupingu mbunge huyo alisema tayari mkandarasi ameshaanza kazi ya ukarabati kwa kiwango cha changarawe baada ya kuipandisha hadhi na kuwa barabara ya mkoa na kupitia barabara hiyo magari makubwa yatawezo kufika ziwa nyasa.

Akijibu maswali ya wananchi kuhusu meli hiyo kufanya safari zake usiku Filikunjombe aliwaambia kuwa atahakikisha ratiba hiyo inabadilishwa kwa sababu ajali na maafa ya meli kutembea usiku ni kubwa sana ukilinganisha na ajali za mchana.

Filikunjombe katika ziara yake ya siku tatu mwambao wa ziwa nyasa iliyoanza Disemba 28 hadi 31 mwaka alitoa mifuko mia moja ya saruji katika sekondari ya makonde, na vifaa vya michezo katika kila kijiji ikiwemo ng,ombe mwenye thamani ya shilingi laki tatu kila kata katika wilaya ya Ludewa.

                      mwisho



No comments:

Post a Comment