Thursday, January 3, 2013



FILIKUNJOMBE AITAKA SERIKALI ITEKELEZE WAJIBU ZAKE   LIGANGA NA MCHUCHUMA.

                   Na Bazil Makungu Ludewa

MBUNGE wa Ludewa katika Mkoa wa Njombe Deo Filikunjombe ameitaka serikali ya Tanzania kutimiza wajibu zake kwa kutekeleza mkataba na makubaliano yaliyoingiwa kati yake na wawekezaji walioko Liganga na Mchuchuma ili kuwezesha miradi hiyo kuanza kwa wakati.

Filikunjombe aliyasema hayo jana alipotembelea maeneo ya uwekezaji ya Liganga na Mchuchuma kujionea mwenyewe hatua iliyofikiwa na wawekezaji hao na kupokea changamoto zinazodhoofisha kasi ya kuanza utekelezaji wa machimbo hayo yanayosubiriwa na kwa hamu na watanzania wengi.

’’’’’ Nimefurahishwa na kasi waliyonayo wawekezaji lakini nimesikitishwa na kasi ndogo ya serikali katika kutekeleza yale yaliyomo kwenye mkataba ikiwa ni pamoja na kutengeneza barabara inayotoka njombe hadi yalipo machimbo ili kupitisha magari na mitambo mikubwa’’’’’ alilalamika Filikunjombe

 HUANG DAXIONG afisa mtendaji wa kampuni ya Tanzania China International Minerals Resouces Limited iliyoundwa kwa ubia kati ya Tanzania na china akitoa taarifa kwa mbunge huyo alisema kasi ya kuanza kwa machimbo ya makaa ya mawe ya mchuchuma na chuma cha Liganga kunadhoofishwa serikali kushindwa kutimiza masharti yaliyomo ndani ya mkataba.

Daxiong aliongeza kuwa wao wanafanyakazi usiku na mchana kulingana mkataba lakini wanashindwa kwa sababu mitambo mikubwa inashindwa kufika eneo la mradi kutokana na serikali ya Tanzania kushindwa kutengeneza barabara za kupitisha mitambo hiyo.

‘’’’’ miradi hii itashindwa kukamilika kwa wakati kutokana na serikali kutotimiza masharti yaliyomo ndani ya mkataba, sisi tunakwenda na wakati lakini tunakumbana na changamoto ambazo mtatuzi ni Serikali ya Jamuhuri ya Tanzania hivyo tunakuomba mbunge utusaidie.’’’’ Alisema Huang

Bw.Daxiong aliyataja makubaliano ya kampuni yake na Serikali kupitia shirika la Taifa la maendeleo(NDC) kuwa  ni pamoja na upanuzi wa barabara kuu kutoka Njombe hadi Mchuchuma ambako ndiko kwenye makaa ya mawe.

Alisema wanashindwa kupitisha mitambo ya kufanyia kazi kutokana na barabara hiyo kuwa nyembamba na madaraja madogo ambapo ni vigumu kupitisha gari zenye tani kubwa katika barabara za wilaya ya Ludewa.

“makubaliano yetu na Serikali ilikuwa ni upanuzi wa barabara haraka iwezekanavyo ili tuweze kufanya kazi ambayo inategemea zaidi kusafirisha mitambo kutoka bandari ya Dar es salaam hadi migodini lakini sisi tumeshaanza kazi Serikali ya Tanzania bado”,alisema Daxiong.

Aidha Daxiong akazitaja changamoto nyingine zinazodhoofisha mradi huo kuwa ni pamoja na urasimu ulioko bandari ya Dar es Salaam katika kuchukua mitambo yao inayotoka nchini China na ucheleweshaji wa vibari vya kufanyia kazi.

Bw.Daxiong alisema urasimu huo ulioko Bandarini pamoja na ucheleweshaji wa vibari umekuwa changamoto kubwa kwao kwani mitambo mingi bado iko bandarini na haijulikani hatima ya tatizo hilo kwani muda unazidi kwenda bila mafanikio.

Alisema suala la vibari lilianza kushughurikiwa kabla ya kusaini mkataba lakini kumekuwa na urasimu mkubwa ambao unawakatisha tamaa wawekezaji hao katika kuifanya kazi hiyo ya uanzishaji wa mgodi kwa wakati muafaka kama walivyotarajia.

Daxiong alimuomba Filikunjombe kuishawishi Serikali ili kuharakisha vibali vya kazi,upanuzi wa barabara na kuondoa urasimu bandarini ili waweze kuondoa mizigo yao haraka pindi inapofika bandarini hapo.

Filikunjombe aliahidi kufuatilia malalamiko hayo lakini akaitaka kampuni hiyo kutokatishwa tamaa na mambo hayo kwani Serikali iko makini ingawa kuna watu wachache wanaozembea kwa maslahi binafsi.

Mkataba unaonesha kuwa kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Limited itawekeza dola za kimarekani bil 3.0 miradi ya Liganga na Mchuchuma na kwamba katika awamu ya kwanza uzalishaji umeme kutoka makaa yam awe ya mchuchuma ni megawati 300 mwaka 2015 na uzalishaji chama cha Liganga  ni tani 500,000 kwa mwaka kuanzia mwaka 2015/16 ambapo awamu ya pili itakuwa kuzalisha umeme kufikia megawati 600 na chuma kufiki tani m.1 kwa mwaka.

                                    Mwisho.

No comments:

Post a Comment