Monday, January 14, 2013

SHEREHE ZA UZINDUZI WA UPANDAJI MITI KITAIFA ZAFANA LUDEWA




                          
MKUU wa Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe Juma  Madaha jana aliongoza Madiwani wote, wakuu wa idara, wananchi na wadau mbalimbali katika uzinduzi wa sherehe za upandaji miti kiwilaya katika kijiji cha Madindo kata ya Ludende na kufanikiwa kupanda Ekari kumi sawa na miche zaidi ya 5450.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo Bw. Madaha alisema maadhimisho haya kitaifa yatafanyika April mosi mwaka huu lakini Ludewa yamefanyika januari 14 kwa kuzingatia hali halisi ya msimu wa mvua katika maeneo mengi ya wilaya hiyo.

‘’’’ sisi kupanda miti leo  ni muda muafaka kabisa kulingana na hali ya hewa ya huku kwa sababu tukisema tungoje mpaka tarehe ya kupanda miti kitaifa mvua kwetu zitakuwa zinaelekea kukatika kwa hiyo upandaji huo utakuwa hauna tija.’’’’ Alisema Bw.Madaha

Aidha Bw.Madaha akaongeza kuwa wilaya yake imeotesha miche zaidi ya milion 4 kwa ajili ya kupanda msimu huu, ambapo kata ya Ludende pekee miche 221,974 imeoteshwa na watu binafsi, vikundi, taasisi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na kuzitaka kata zingine zenye mwamko mdogo kujifunza ili kujiletea maendeleo yao.

‘’’’ ndugu wananchi leo ni siku ya uzinduzi wa upandaji miti kiwilaya, hii ina maana kuwa upandaji wa miti ulishaanza na utaendelea  baada ya hapa mpaka hapo mvua zitakapokaribia kukatika, Kila mwananchi anatakiwa kujiwekea malengo ya kupanda miti ya kutosha ili kufikia lengo.’’’alisisitiza Bw.Madaha.

Naye Fidelis Lumato  Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa akawataka wananchi kuacha tabia ya kuchoma moto hovyo na kuacha kutegemea kilimo cha mazao ya mahindi pekee katika kujikwamua na umaskini badala yake wageukie upandaji miti na kutumia mazao ya mbao kujiondoa kwenye wimbi la umaskini wa kipato kwani miti haihitaji pembejeo.

Bw.Kimato akaongeza kuwa mkakati wa kupunguza umaskini hauwezi kufanikiwa bila kuzingatia suala la kuhifadhi mazingira kwa kuwa wilaya bado ina uoto mzuri wa asili kwasababu misitu ya asili haijaharibiwa ukilinganisha na maeneo mengine nchini.

Uharibifu wa mazingira unaoikabili wilaya ya Ludewa ni pamoja na uchomaji miti, na misitu unaosababisha mmomonyoko wa udongo na mafuriko, kulima kwenye vyanzo vya maji na mabonde chepechepe ambapo matokeo yake ni kukauka kwa vyanzo ya maji miche na chemichemi.

Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi Afisa ardhi na mali asili wilaya ya Ludewa Gilbert Ngailo alisema lengo la kufanyia uzinduzi wa kupanda miti katika kata ya Ludende ni kutokana na hamasa na mwitiko walionao wananchi wa kata hiyo hasa kwenye suala la upandaji miti ambapo kila mwananchi ana ekari zaidi ya moja.

‘’’’ dawa ya kukomesha uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto kichaa itapatikana muda si mrefu ambapo halmashauri itaunga sheria ndogondogo kwa ajili ya kumtaka kila mwananchi kupanda miti kwa kiwango cha kima cha chini ekari mbili kufanya hivyo kila mtu atakuwa mlinzi wa mwenzake.’’’’ Alisisitiza Ngailo

Ngailo aliyataja maeneo mengine yenye mashamba ya miti ya halmashauri kuwa nipamoja na shamba la miti lenye ekari 20 za miti ya mikaratasi  ambayo tayari imeanza kuvunwa,Mlangali yenye miti hekta 61 aina ya milingoti na ekari 10, kijiji cha Ilininda ekeri 10, Utiriri ekari 10 na madindo ekari zaidi ya 102 sawa na hekta 40.
                     mwisho

 

No comments:

Post a Comment