Na Bazil Makungu Ludewa
WANAWAKE hasa akina mama wajawazito katika kata ya Luana Wilayani
Ludewa katika mkoa wa Njombe wanalazimika kutembea kwa miguu kwa umbali wa
zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma ya afya katika hospitari ya wilaya ya
Ludewa huku wengine wakijifungulia njiani imefahamika.
Akitoa
taarifa ya zahanati hiyo iliyopo katika kijiji cha Luana katika kikao
kilichoandaliwa na shirika la Daraja linalofanya utafiti katika idara ya Afya
kwa kuwakutanisha watoa huduma katika zahanati za serikali zilizoko pembezoni Afisa
mtendaji wa kijiji cha Luana Bw.Ladislaus Morani alisema wananchi wananlazimika
kutembea umbali mrefu kufuata huduma katika hospitari ya wilaya ya Ludewa kwa
miguu.
‘’’’ wanaoteseka sana ni akina mama
wajawazito na watoto ambao huduma yao ya kliniki haipatikani katika zahanati hiyo
inayomilikiwa na kanisa katoliki jimbo
la njombe kama sasa hivi hakuna dawa kabisa wajawazito hutembea kwa miguu km 10,
na kwa waliona uwezo husafiri kwa pikipiki (Bodaboda) usafiri ambao ni hatari
sana.’’’’ Alisema Morani
Akizungumza
katika kikao hicho cha wadau wa Afya kutoka katika zahanati nne za Ludende,
Luana,Lihagule na Mkomang’ombe kaimu Mkurugenzi wa shirika la Daraja lenye makao
yake makuu mkoani Njombe Simon Mkina alisema shirika lake linafanya kazi ya
kutoa msukumo kwa Viongozi na watendaji wa Serikali lengo likiwa kutoa huduma
stahiki katika jamii.
Alisema
kumekuwa na changamoto kubwa katika sekta ya afya hivyo tafiti inayofanywa na
shirika la Daraja imeonesha kuibua mambo
mengi katia zahanati na vituo vya afya vilivyoko vijijini
kutokana na maeneo mengi kusahaulika katika huduma hizo.
“tumeanza
kufanya tafiti katika mikoa miwili ya Iringa na Njombe na matokeo yatakayopatikana
katika mikoa hii tunaamini ni ya nchi nzima na baada ya hapo tutatoa taarifa
katika Halmashauri husika ili wajirizishe na taarifa yetu na baada ya hapo
taarifa hizo zitatolewa katika vyombo mbalimbali vya habari ili kuujulisha umma
nini tunakifanya”,alisema Bw.Mkina.
Mkina
alisema mpango huu utafanikiwa ikiwa
kila mwananchi na mdau wa Afya ataeleza ukweli kuhusiana na huduma zitolewazo
ambapo watahitaji kujua upatikanaji wa dawa,wafanyakazi wa sekta ya afya kama
wanakidhi mahitaji,upatikanaji wa maji safi katika zahanati,vyombo vya usafiri
kwa wagonjwa na mapungufu katika nyumba za wafanyakazi na motisha zao.
Akifungua kikao hicho Mganga mkuu wa
wilaya Ludewa Dakt.Hapines Ndossi alisema
wilaya yake inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo utafiti huo
utabaini,lakini changamoto kubwa anayokabiliana nayo ni upungufu wa wafanyakazi
ambapo wamekuwa wakiacha kazi kutokana na mazingira ya kazi kuwa magumu.
Dr.Ndossi
alisema wilaya ya Ludewa inazaidi ya vituo vya Afya 50 ambavyo vinachangamoto
ya upungufu wa watumishi na nyumba za kuishi watumishi hali ambayo inawakatisha
tama wananchi waliojitolea nguvu zao kuvijenga vituo hivyo.
Kuhusu
zahanati ya mishioni ya Luana Dr Ndossi alisema kuwa mkataba kati ya serikali
na mmiliki wa zahanati hiyo umeshaandaliwa kinachosubiriwa ni kutiliana saini
kati ya serikali na mmiliki kupitia mpango wa Public Private Partinership
(PPP).
Naye diwani
wa kata ya Luana Thomaso Haule akaliambia gazeti hili kuwa kutokana na kero
inayowakabili wananchi tayari tofali zaidi ya laki moja zimeshachomwa kwa ajili
ya ujenzi wa zahanati ya serikali na kwamba wananchi wanatarajia kuanza ujenzi
mwezi mei mwaka huu mvua zitakapopungua.
Alisema
Halmashauri ya wilaya inampango wa kutekeleza sera ya Serikali ambayo imelenga
kujenga zahanati kwa kila kijiji ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito
vinavyotokana na kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma ya Afya.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment