Na Bazil Makungu Ludewa
MKUU wa Wilaya ya
Ludewa katika Mkoa wa Njombe Juma Madaha amekemea vikali pepo mbaya wa uchawi
na ushirikina vinavyoendelea kuandama wananchi wa Ludewa kijijini na kupelekea
watu kuogopa kutangulia kuingiza umeme majumbani mwao kwa hofu ya kugeuzwa
kafara.
Mkuu wa wilaya ya
Ludewa akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, makamu mwenyekiti wa Halmashauri
ya wilaya Monica Mchiro ambaye pia ni
diwani wa kata ya Ludewa na wakuu wa idara mbalimbali walikwenda katika kijiji
hicho kuhamasisha na kukemea uvumi ulioenezwa na baadhi ya watu kuwa mtu
atakayekuwa wa kwanza kuingiza umeme atatolewa kafara ndipo wengine wataanza
kuingiza majumbani mwao.
Madaha akawaambia
wakazi wa kijiji hicho kuwa serikali haiamini uchawi na kuwataka wale wote
wanaojihusisha na mambo ya ushirikina waache mara moja kuwatishia watu
wanaohitaji kujiletea maendeleo ya kweli.
’’’’’ kama vitendo
vya vitisho vitaendelea kuleta hofu miongoni mwa wananchi, baada ya kilimo
kupungua nitafika kijijini hapa na kusimamia upigaji wa kura za siri kuwabaini
wachawi na kutengwa kwa kujengewa kijiji chao ili wakaendelee kulogana wenyewe
na kupisha maendeleo kwa wenzao.’’’’ Alionya Madaha na kusisitiza
Akitoa taarifa kwa
mkuu wa wilaya hiyo meneja wa shirika la umeme tawi la Ludewa Peter Molel
alisema serikali imetoa punguzo la uingizaji umeme majumbani na kufikia ghrama
ya shilingi 177,000 badala ya shilingi 465,000 zilizokuwa zikitolewa awali.
Alisema pamoja na
serikali kutoa ofa hiyo bado kasi ya uingizaji umeme ni ndogo ambapo hadi sasa
ni wateja 795 walioingiza na kwamba mitambo na mashine zilizopo zinauwezo wa
kufua kilowati 1270 lakini ni kilowati 100 tu ndizo zinazotumika kwa hiyo serikali
inaendesha mitambo kwa hasara.
Hofu hiyo imetanda
kufuatia historia ya kijiji hicho kuandamwa na matukio mengi ya vifo vya
kutatanisha hasa kwa vijana vinavyotokana na mazingira ya ajabu kama kupigwa
radi na kufa na baada ya kuzikwa wanaanza kuonekana wakirandaranda mitaani na
kuhatarisha usalama.
Erick Kidulile na
Romanus Haule wao wakaenda mbali zaidi na kumwambia mkuu wa wilaya kuwa vijana
wamechoshwa kunyanyaswa na wachawi sasa hivi watu wanalazimika kulala saa mbili
kama kuku kwa hofu kuwa wakitembea wanakutana na majini tena ambao wanajua kuwa
walishazikwa.
‘’’’’ Mheshimiwa mkuu
wa wilaya tunashukuru kwa kuja kwako, lakini inasikitishwa hivi inawezekanaje
mtu aliyekufa na kuzikwa baada ya siku mbili tatu anaonekana akipita mitaani na
kwenye nyumba za watu akiomba chakula?’’’’ Aliuliza Erick huku akionekana
mwenye majonzi
Stanley Gowele ni
katibu wa mbunge wa Ludewa Filikunjombe akitoa salaam za mbunge kwa wananchi wa
kijiji cha Ludewa(K) akawatoa hofu wakazi hao na kuwambia kuwa mbunge
anawathamini na ndiyo maana amehakikisha umeme unawafikia kwa sababu ni haki
yao na kuwataka wautumie umeme huo kwa sababu utachochea kasi ya maendeleo na
kuondokana na umaskini wa kipato.
Mradi wa umeme Ludewa
mjini ulianza mwaka 2006 na kuwashwa julai 2, 2008 na jumla ya shilingi milioni
233,266,425.60 zimetumika kufikisha umeme katika kijiji cha Ludewa (K) ikiwa ni
gharama ya miundombinu ya laini kubwa na ndogo.
mwisho
No comments:
Post a Comment