Monday, March 24, 2014

WATAKA SERIKALI IHARAKISHE KUPIMA VIWANJA KATIKA MIJI MIDOGO ILIYOTANGAZWA.





             Bazil Makungu 

WANANCHI wa kata ya Lugarawa katika wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe wameitaka serikali kuharakisha mchakato wa upimaji wa viwanja katika miji midogo iliyotangazwa hivi karibuni ili waanze kuviendeleza kwa kujenga nyumba za kisasa sanjari na kuingizia halmashauri mapato.

Wakizungumza na gazeti hili walisema kukamilika kwa mchakato huo kutapunguza migogoro ya ardhi inayoendelea kuwakumba wananchi wa miji hiyo midogo kutokana na watu kuvamia ardhi ya wengine kwa visingozio vya mipaka. 

Ali Ponda mwenyekiti wa kijiji cha Mdilidili katika kata ya Lugarawa kwa upande wake alisema zoezi la upimaji viwanja kwa wakati itarahisisha na kuainisha maeneo ya makazi, malisho, maeneo ya hifadhi na viwanja ya michezo.

Naye Afisa mipango miji wilaya ya Ludewa Isack Makinda alisema eneo la mipango miji la Lugarawa ni miongoni mwa maeneo matano ya kimpango miji katika wilaya ya Ludewa na kuyataja kuwa ni pamoja na kata ya Ludewa, Mlangali, Mawengi na Manda. 

Makinda aliongeza kuwa eneo la kijiji cha Mdilidili na Lugarawa lilitangazwa kwenye gazeti la serikali namba 217 na kuchapishwa septemba 7 mwaka 2001 baada ya kupitia hatua zote za kisheria.

Afisa ardhi alizitaja changamoto zilizojitokeza katika mchakato huo kuwa ni pamoja na ongezeko la ujenzi holela kwenye makazi ya watu,ongezeko la migogoro ya ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama uwekezaji, miundombinu na ugomvi wa mipaka na ardhi huru kwa ajili ya huduma za jamii kama shule zahanati makaburi na nyumba za ibada.

Changamoto zingine ni ongezeko la watu wanaohitaji hati za viwanja, uvamizi wa ardhi kwenye vyanzo vya maji, kukosekana kwa maeneo ya uwekezaji kama vile viwanda na biashara.

Makinda alizitaja faida za kupima ardhi kuwa ni pamoja na wananchi kukatiwa hati miliki na kuongezeka kwa thamani ya ardhi, kupunguza ujenzi holela na migogoro, kuwepo na ardhi kwa ajili ya matumizi ya umma.


No comments:

Post a Comment