Wednesday, August 6, 2014

FILIKUNJOMBE ATIMUA MKURUGENZI, WAKUU WA IDARA KATIKA MKUTANO WA HADHARA. WANANCHI WAZOMEA NA KUSEMA WANASUBIRI VIFAA VYA ZAHANATI YAO.



Na Bazil Makungu Ludewa

MBUNGE wa jimbo la Ludewa katika mkoa wa Njombe Deo Filikunjombe jana alilazimika kumfukuza kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya na wakuu wa idara baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu vilipo vitanda, magodoro na mashuka vifaa alivyovinunua yeye mwenyewe mwaka mmoja uliopita kwa ajili ya zahanati ya Ihanga iliyopo kata ya Mlangali.

Awali Filikunjombe alikataa kufanya mkutano katika uwanja uliokuwa umeandaliwa badala yake akamtaka mwenyekiti wa kijiji cha mlangali ndani kuwaita wananchi na kufungua mkutano kwenye viwanja vya zahanati hiyo

Katika ziara yake ya wiki moja ya kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake Filikunjombe alifuatana na kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Horace Kolimba akiwemo kaimu mganga mkuu na wakuu wa idara za kilimo, maji na ujenzi.

Hali ya hewa ilianza kuchafuka katika mkutano baada ya Filikunjombe kukagua zahanati na kugundua mapungufu mengi ikiwemo ukosefu wa vitanda vya kupumzikia wagonjwa na akina mama na kitanda cha kujifungulia vifaa ambavyo alivinunua mwenyewe na kutoa fedha ya usafiri na kuikabidhi halmashauri ya wilaya kwa ajili ya kupeleka katika zahanati lakini wamekaa navyo huku wananchi wakiendelea kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi Horace Kolimba baada ya kukosa majibu alimwomba Filikunjombe ampe wiki moja ili aweze kuvifikisha vifaa hivyo lakini kwa mbunge ilikuwa vigumu kukubali ombi hilo na ndipo hatua ya kuwafukuza ilitimia na kusimamisha mkutano kwa muda mpaka vifaa vyao vitakapoletwa.

‘’’ wananchi mmejionea wenyewe wameshindwa kutoa majibu mbele yenu sasa hatuendelei na mkutano waondoke hapa wakalete vifaa vyetu ndipo mkutano uanze hatuwezi kukaa hapa tunapiga siasa wakati huduma za zahanati zimekaliwa na watendaji, serikali yetu na chama cha mapinduzi inaonekana haifanyikazi kwa sababu ya watendaji wabovu kwenye jimbo langu siwezi kuwavumilia.’’’ alilalamika filikunjombe

Umbali kutoka ilipo zahanati ya Ihanga Mlangali na makao makuu ya wilaya ni takribani kilometa 75 lakini kutokana na msimamo wa mbunge wao wananchi walikubali kusubiri bila kuchoka huku wakitumbuiza na kucheza ngoma za asili mpaka vifaa vyote vilipofika na kuhesabiwa na kisha kukabidhiwa kwao.

‘’’ mafuta ya gari la mkurugenzi na posho yake havikosekani katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa lakini mafuta ya kuleta vifaa katika zahanati kwa kipindi cha mwaka mzima wanasema hayapo na sasa hivi tunavyoongea mkurugenzi Wiliam Waziri yuko mbeya kuzifuata posho. Alisikitishwa filikunjombe

Diwani wa kata hiyo kupitia chadema Faraja Mlelwa alimpongeza mbunge huyo kwa kuchapa kazi na kuwatumikia wananchi kwa moyo wote bila ubaguzi na kusema kuwa katika suala la maendelea lazima tuweke itikadi zetu pembeni na kuahidi kutoa ushirikiano.
mwisho





No comments:

Post a Comment